Elimu ya mtaani na maajabu yake katika mafanikio ya ndoto za watu.
Ndugu msomaji wangu naamini kuwa umzima wa afya popote pale ulipo na unaendelea vyema na shughuli zako za kila siku katika juhudi za kuyajenga mataifa yetu. Yamkini hapo unapoisoma makala hii unatumia mojawapo ya chombo cha mawasiliano kama simu, kompyuta au hata kishikwambi.
Bila kupepesa macho nikupongeze wewe hapo unayeendelea kuyasoma maneno haya kwa kuwa umeamua kuchukua maamuzi sahihi kabisa na kukitumia chombo chako cha mawasiliano si tu kwa kuwatafuta ndugu, jamaa na marafiki bali pia kama darasa huru la kukuongezea maarifa na elimu ya mtaani kwa ujumla.
KUSOMA SIYO WAJIBU WA WANAFUNZI MASHULENI NA VYUONI TU
Kipekee ningeomba kutoa wito kwa vijana WOTE kuachana na dhana ya kuamini kuwa jukumu la kusoma lipo tu kwa wanafunzi waliopo mashuleni na vyuoni laa hasha bali watu wote hasa vijana tunatakiwa kupenda kusoma vitabu, majarida, makala mbali mbali, nk. Kwani kwa kusoma mara kwa mara tutajifunza mambo mengi yatakayotuwezesha kuyakabili matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye maisha yetu ya kila siku. Japokuwa limekuwa ni suala gumu kwa vijana wengi kujikita katika kusoma mambo yenye manufaa ya moja kwa moja kwenye maisha yetu. Badala yake tumekijikita katika kusoma kwa nguvu zote mambo ambayo hayana faida kubwa kwetu.
Kuthibitisha hilo fuatilia kwa karibu ni taarifaa gani zinazofuatiliwa na vijana wengi kwenye magazeti, kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii na vyazo vingine vya habari. Kimsingi utakuta habari za udaku, michezo, burudani na vichekesho vikichukua nafasi kubwa na kupata wafuatiliaji wengi ambapo wengi wao ni vijana. Simaanishi kwamba hatutakiwi kufuatilia taarifa za kijamii hapana, bali tunatakiwa kuifahamu vizuri sana jamii yetu kwa kusoma taarifa na matukio ya kila siku yanayoendelea ili kuwa na uwezo wa kuishi kulingana na matukio yaliyopo kwenye jamii zetu.